Ofisi ya Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa imesema katika taarifa fupi iliyochapishwa na shirika la habari la Reuters kwamba: “Vitendo vya kigaidi havina nafasi katika kanuni za makundi ya muqawama. Uongo na udanganyifu haviwezi kubadili nafasi ya mlalamikaji kuwa ya mtuhumiwa.”
Shirika la habari la Reuters liliripoti siku ya Alhamisi kwamba waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Israel, Israel Katz, alimuonya mwenzake wa Ufaransa Stephane Sejourne kuhusu kile alichodai kuwa eti majaribio ya kufanya mashambulizi dhidi ya Waisraeli wakati wa michezo ya Olimpiki.
Madai hayo ya utawala bandia wa Israel yamekuja wakati kampeni ya kimataifa ikianzishwa kuwapiga marufuku wanariadha Waisraeli katika michezo hiyo, kutokana na mauaji ya kimbari yanayoendelea kutekelezwa na utawala huo katika Ukanda wa Gaza ambayo yamesababisha vifo vya Wapalestina 39,175 wengi wao wakiwa wanawake na watoto tangu Oktoba mwaka jana.
Wanaharakati wanaoiunga mkono Palestina wameanzisha kampeni ya kuwashinikiza waandaaji kuwazuia wanariadha wa Israel kushiriki katika michezo hiyo inayotarajiwa kuanza leo.
Wanaharakati hao wamesisitiza kwamba "kusherehekea maadili ya kibinadamu ya Olimpiki kunapingana na vitendo vya kikatili na mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na Israel dhidi ya Wapalestina."
342/